UN yaeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko ya Congo DR
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameeleza wasiwasi wake kuhusu ghasia na machafuko ya kisiasa nchini humo.
Maman Sidikou ambaye alikuwa akihutubia kikao cha wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu machafuko ya kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kusema kuwa, mapigano na ghasia zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan katika eneo la Kasai na kwamba wahusika wa machafuko na ukatili huo hawachukuliwi hatua za kisheria.
Sidikou ameashiria makubaliano ya Disemba mwaka jana kati ya serikali ya Kinshasa na wapinzani wake na kusema kuwa, kwa sasa kuna udharura wa kutangazwa jedwali ya wakati wa uchaguzi, kutengwa bajeti yake na kuchukuliwa hatua za dharura za kudhamini haki za watu ili kufanikisha mchakato wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya Congo inawajibika kuitisha chaguzi za Rais, Bunge na serikali za kieneo hadi kufikia Disemba mwaka huu.
Machafuko ya ndani nchini Congo yalipamba moto baada ya kuahirishwa uchaguzi wa rais na kile wapinzani wanachosema ni nia ya Rais Joseph Kabila ya kung'ang'ania madaraka ya nchi hiyo.