Mauaji ya watu 276 katika shambulio la kigaidi nchini Somalia
Mripuko wa lori lililotegwa bomu ndani yake uliua watu wasiopungua 276 mjini Mogadishu, Somalia siku ya Jumamosi jioni.
Kwa mujibu wa polisi ya Somalia, mripuko huo ulitokea karibu na hoteli moja mjini humo. Shambulio hilo limetokea baada ya hujuma kadhaa za kigaidi katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, huku likiwa ndilo kubwa zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha hivi karibuni. Miripuko huo umejiri katika hali ambayo, mashambulizi ya kigaidi na migogoro ya kisiasa, matatizo ya kiuchumi ukiwemo umasikini na ukosefu wa ajira na kadhalika ukame ambao umeyaathiri maeneo mengi ya taifa hilo la Pembe ya Afrika, ni kati ya matatizo makubwa ambayo yanaendelea kuisakama Somalia kwa sasa.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Somalia imepata mabadiliko kadhaa ya kisiasa. Kufanyika uchaguzi wa rais ikiwa ni baada ya kupita miaka kadhaa na kadhalika kuundwa baraza la mawaziri, ni miongoni mwa mabadiliko hayo ya kisiasa. Tangu alipoingia madarakani Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia maarufu kwa jina la 'Farmajo' alitangaza kipaumbele cha kwanza kwa serikali yake kuwa ni kudhamini usalama na amani nchini humo, hata hivyo mwenendo wa sasa unaonyesha kwamba kiongozi huyo hajafanikiwa katika uwanja huo.
Francisco Caetano Madeira, mwakilishi maalumu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika masuala ya Somalia anaamini kwamba, kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab bado linaendelea kufanya mauaji huko Somalia, huku likimshambulia kila mtu anayejaribu kukabiliana nalo. Kundi la ash-Shabab ambalo ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah tokea mwaka 2012, lilikuwa likidhibiti maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia lakini lilipokonywa maeneo hayo muhimu, ikiwemo miji mikubwa ambayo ilikuwa mikononi mwa wanachama wa genge hilo mwaka 2015 kufutia operesheni nzito zilizofanywa na jeshi la Somalia kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM). Tangu wakati huo kundi hilo limefanya mashambulizi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya Somalia na hata katika ardhi ya nchi jiraji.
Kuongezeka mashambulizi ya kundi la ash-Shabab nchini Somalia kunajiri katika hali ambayo, siku chache zilizopita Abdirashid Abdullahi Mohamed, Waziri wa Ulinzi na Ahmed Mohamed Jimale, kamanda wa jeshi la nchi hiyo walitangaza kujiuzulu. Baadhi ya weledi wa mambo walitaja sababu ya viongozi hao wa kijeshi kujiuzulu kuwa ni kufeli kwa siasa za serikali ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia za kupambana na kundi la kigaidi la ash-Shabab na kadhalika kuongezeka hujuma za kigaidi za genge hilo. Kupambana na kundi hilo na kung'oa mizizi yake, kuimarisha usalama na amani, kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii ukiwemo ukosefu wa ajira, umasikini na ukame, ni kati ya vipaumbeloe ambavyo vimekuwa vikifuatiliwa na serikali ya Mogadishu tangu ilipoingia madarakani.
Hata hivyo hadi sasa haijaweza kudhibiti hali ya mambo. Michael Keating, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia sambamba na kuashiria hali mbaya ya kibinaadamu na hatari ya ukame vinavyoikabili nchi hiyo kwa sasa, ametaka kuchukuliwa hatua za dhati kwa ajili ya kutatuliwa matatizo hayo. Kwa kuzingatia tatizo hilo, inaonekana kuwa kabla ya mambo mengine yote serikali ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed inatakiwa kwanza iondoe tofauti zilizopo za kisiasa na kikabila na kutekeleza mipango ya kuimarisha uthabiti wa kisiasa na usalama nchini Somalia, suala ambalo litasaidia kutatua matatizo hayo na hivyo kurahisisha njia ya kufikia malengo yake.