Kamanda wa zamani al-Shabaab alaani mashambulizi ya Mogadishu
(last modified Wed, 18 Oct 2017 02:50:37 GMT )
Oct 18, 2017 02:50 UTC
  • Kamanda wa zamani al-Shabaab alaani mashambulizi ya Mogadishu

Aliyekuwa Naibu Kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na pia msemaji wa zamani wa genge hilo Mukhtar Robow amelaani vikali shambulizii la kigaidi lililoua watu zaidi ya 300 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu Jumamosi iliyopita.

Robow ambaye pia anajulikana kwa jina la Abu Mansur sambamba na kutowa damu kwa ajili ya kuwasaidia manusura wa hujuma hiyo, amelitaja shambulio hilo kuwa ni ukatili na kitendo kinachokiuka mafundisho ya Kiislamu. Vilevile amewataka magaidi wanaofanya unyama huo dhidi ya watu wasio na hatia hususan watoto wadogo na wanawake watubu na washikamane na mafundisho sahihi ya Uislamu.

Amesema: "Takriban miaka 10 iliyopita, niliwataka viongozi wenzangu wa al-Shabaab kutofanya mashambulizi ya umwagaji damu dhidi ya raia lakini hawakusikia. Walipanga njama ya kuniua kutokana na ukosoaji wangu dhidi ya idiolojia zao za upotofu."

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Garowe, nchi moja miongoni mwa nchi zilizotuma wanajeshi wao Somalia katika kikosi cha Amisom inapanga kumpa Mukhtar Robow uungaji mkono wa silaha na kilojistiki, aongoze genge litakalopambana na al-Shabaab.

Robow alipokuwa msemaji wa al-Shabaab

Agosti mwaka huu, Robow alijisalimisha kwa jeshi la Somalia katika mji wa Hudur, kusini magharibi mwa nchi, miezi miwili baada ya Marekani kuondoa jina lake katika orodha ya magaidi hatari inaowasaka sambamba na kufuta zawadi ya Dola milioni 5 kwa yeyote ambaye angemkamata au angetoa taarifa ya kupelekea kukamatwa kwake. 

Ingawaje hakuna kundi lolote la kigaidi lililotangaza kuhusika na mauaji hayo ya raia wasio na hatia mjini Mogadishu siku ya Jumamosi, lakini duru za kiusalama zimedokeza kuwa, yumkini genge la kitakfiri la al-Shabaab ndilo lililofanya ukatili huo.

Tags