Waislamu Nigeria waandamana wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35894-waislamu_nigeria_waandamana_wakitaka_sheikh_zakzaky_aachiliwe_huru
Waislamu nchini Nigeria wameendeleza maandamano wakitaka Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 23, 2017 14:01 UTC
  • Waislamu Nigeria waandamana wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Waislamu nchini Nigeria wameendeleza maandamano wakitaka Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.

Taarifa zinasema Waislamu katika jimbo la Sokoto  kaskazini magharibi mwa Nigeria waliandamana katika miji yote ya jimbo hilo siku ya Jumapili wakitaka Sheikh Zakzaky, ambaye pia ni kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia aachiliwe huru. Duru zinaarifu kuwa maandamano hayo yalikuwa ya amani lakini maafisa wa usalama waliwashambulia waandamanaji kwa silaha na kuwatawanya. Walioshuhudia wanasema polisi walishambulia kituo kimoja cha Waislamu wa madhehebu ya Shia na kumkamata mtu mmoja.

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu. Hata hivyo licha ya mahakama kutoa hukumu ya kutaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo, bado vyombo vya usalama vya Nigeria vinaendelea kumshikilia katika korokoro isiyojulikana huku ripoti zikifichua kwamba hali yake ya kiafya ni mbaya.

Polisi Nigeria wamewarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakifanya maandamano ya amani mara kwa mara ambapo wamekuwa wakisisitiza juu ya udharura wa serikali ya Nigeria kuheshimu sheria na hukumu ya mahakama ya nchi hiyo iliyotaka kuachiwa huru kiongozi wao.