UN: Watu milioni 3 wanakabiliwa na njaa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36042-un_watu_milioni_3_wanakabiliwa_na_njaa_kongo_dr
Mpango wa Chakula Duniani WFP umesema watu zaidi ya milioni 3 wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutoka na njaa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2017 04:32 UTC
  • UN: Watu milioni 3 wanakabiliwa na njaa Kongo DR

Mpango wa Chakula Duniani WFP umesema watu zaidi ya milioni 3 wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutoka na njaa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkuu wa WFP David Beasley ametoa wito wa kutumwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu hao wa Kongo DR, hususan watoto wadogo.

Amesema mamia ya watoto wadogo watapoteza maisha katika miezi michache ijayo katika nchi hiyo ya Kiafrika iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kunusuru maisha yao.

Mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa, hali ya kibinadamu katika mkoa wa Kasai ni ya kutisha, ambapo tayari watoto wengi wameaga dunia, huku wengine wengine wakikabiliwa na utapiamlo.

Baa la njaa linashuhudiwa Kongo licha ya utajiri mkubwa wa maliasili nchini humo

Ameongeza kuwa, kwa sasa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa lina asilimia moja tu ya msaada wa chakula unaohitajika kwa ajili ya mamilioni ya Wakongomani.

Machafuko na ukosefu wa amani vinaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Kongo DR kwa zaidi ya miaka ishirini sasa.