'Polisi Kenya wameshaua watu 36 katika machafuko ya uchaguzi'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36097-'polisi_kenya_wameshaua_watu_36_katika_machafuko_ya_uchaguzi'
Shirika moja la haki za binadamu la Kenya limetoa ripoti na kusema kuwa, zaidi ya watu 36 wameshauliwa na polisi tangu tarehe 11 Agosti siku yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi wa kwanza wa rais nchini Kenya hadi hivi sasa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 01, 2017 12:47 UTC
  • 'Polisi Kenya wameshaua watu 36 katika machafuko ya uchaguzi'

Shirika moja la haki za binadamu la Kenya limetoa ripoti na kusema kuwa, zaidi ya watu 36 wameshauliwa na polisi tangu tarehe 11 Agosti siku yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi wa kwanza wa rais nchini Kenya hadi hivi sasa.

Gazeti la kila siku la Daily Nation la nchini Kenya limeripoti habari hiyo na kulinukuu shirika la haki za binadamu la Independent Medico Legal Unit (IMLU) likisema leo Jumatano kwamba, watu 23 waliuliwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Agosti na 13 wameuawa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Shirika hilo limeongeza kwamba polisi wa Kenya wameua watu hao kwa kutumia nguvu za ziada wakati wa kuzima machafuko ya wapinzani.

Machafuko ya uchaguzi Nairobi Kenya

 

Shirika la haki za binadamu la IMLU pia limesema, limerekodi vitendo kadhaa vya uvunjaji wa haki za binadamu vilivyofanywa na Jeshi la Polisi la Taifa la Kenya katika kipindi cha chaguzi hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Peter Kiama aidha amehoji namna vikosi vya ulinzi vya Kenya vinavyoratibu mambo na kusema kuwa, katika maeneo mengi kumetumwa maafisa wapya wa polisi bila ya kujulishwa maafisa wa polisi waliokuwa wanahudumu kwenye vituo hivyo.

Ni hivi majuzi tu ambapo jeshi la polisi nchini Kenya lilikabiliana na magenge ya wafanya fujo katika eneo la Kawangware jijini Nairobi ambapo magenge hayo yalikuwa yanapora maduka na nyumba za raia na kuchoma moto maeneo ya biashara.

Machafuko ya uchaguzi nchini Kenya

 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, magenge hayo ambayo yalidaiwa kufanya fujo kulalamikia marudio ya uchaguzi wa rais wa siku ya Alkhamisi Oktoba 26, 2017, waliwashambulia na kuwajeruhi vibaya raia.

Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa, wameona watu watatu wakiwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika fujo hizo wakiwemo wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Ndurarua ambao walijeruhiwa vibaya katika fujo hizo.