Kuendelea uchukuaji hatua za kikatili na za ukandamizaji dhidi ya Waislamu Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36236-kuendelea_uchukuaji_hatua_za_kikatili_na_za_ukandamizaji_dhidi_ya_waislamu_nigeria
Katika muendelezo wa hatua kandamizi zinazochukuliwa dhidi ya Waislamu wa Nigeria, watu wasiopungua watatu wameuliwa baada ya polisi kuwafyatulia risasi wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 07, 2017 23:18 UTC
  • Kuendelea uchukuaji hatua za kikatili na za ukandamizaji dhidi ya Waislamu Nigeria

Katika muendelezo wa hatua kandamizi zinazochukuliwa dhidi ya Waislamu wa Nigeria, watu wasiopungua watatu wameuliwa baada ya polisi kuwafyatulia risasi wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Mnamo mwaka huuhuu pia askari polisi wa Nigeria wamewafyatulia risasi Waislamu waliokuwa wakiandamana kwa amani kuelekea kwenye makaazi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky sambamba na kukaribia Arubaini ya Imam Hussein (as).

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky

Hatua za ukandamizaji na mauaji ya Waislamu wa Nigeria yameshadidi katika miaka ya karibuni hususan mwishoni mwa mwaka 2015 wakati vikosi vya jeshi vilipovamia na kushambulia Husseiniyyah ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah mjini Zaria katika jimbo la Kaduna. Katika shambulio hilo, mamia ya Waislamu waliuawa; na Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mke wake walitiwa nguvuni. Tangu wakati huo hadi sasa, mwanazuoni huyo angali yuko mahabusu.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, akiwa amejeruhiwa vibaya kabla ya kutiwa nguvuni na askari wa jeshi la Nigeria

Ijapokuwa hukumu ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky ilikwisha tolewa na Mahakama Kuu ya Nigeria tangu muda mrefu nyuma, sio tu hajaachiwa huru, lakini mashinikizo ya Waislamu wa nchi hiyo dhidi ya hatua ya kuendelea kumshikilia kiongozi huyo wa kidini nayo pia yameongezeka. Katika miaka ya karibuni, vikosi vya jeshi na vya usalama vya Nigeria vimekuwa vikipinga kufanyika mikusanyiko na maandamano yoyote ya amani ya Waislamu na vimekuwa vikitumia mkono wa chuma kukandamiza washiriki wa mikusanyiko ya aina hiyo.

Mas'ud Shadjareh, mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu

Mas'ud Shadjareh, mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za binadamu yenye makao yake mjini London, Uingereza ameizungumzia hali hiyo kwa kusema: "jinai za vikosi vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo inapasa zifikishwe na kuzungumziwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa sababu serikali ya Nigeria inalifumbia macho jambo hilo.

Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria na ukatili na ukandamizaji wanaofanyiwa vinajiri katika hali ambayo, kwa miaka na miaka jamii ya Waislamu hao imekuwa ikiishi kwa amani na utulivu na wananchi wenzao. Wachambuzi wa masuala ya nchi hiyo wanaitakidi kuwa hali inayoshuhudiwa hivi sasa ni matokeo ya mashinikizo na utekelezaji wa sera mpya ambayo maelekezo yake yanatoka kwenye baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya nchi za bara la Afrika hususan Nigeria, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu barani humo.

Kwa miaka kadhaa sasa baada ya kufeli na kugonga mwamba sera za utawala wa Kizayuni katikia eneo hili la Mashariki ya Kati, utawala huo haramu umekuwa ukitafuta fursa ya kujipenyeza katika nchi nyingi za Afrika kwa ajili ya kustawisha uhusiano na kufaidika na utajiri wa maliasili za nchi hizo. Nayo Saudi Arabia pamoja na baadhi ya nchi nyengine za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zimeibuka na muelekeo mpya wa kutaka kuwafarakanisha Waislamu na kupanua satua zao katika nchi za Waislamu barani Afrika. Miongoni mwa hatua zao ni kuyaunga mkono makundi yanayobeba silaha barani humo na kuyapatia silaha na zana kwa ajili ya kukabiliana na Waislamu. Kuhusiana na suala hilo, Sheikh Adam Husu, mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema: "serikali ya Nigeria inaathiriwa na ushawishi wa siasa za utawala wa Aal Saud, Marekani na utawala wa Kizayuni; na wote pamoja wanakula njama dhidi ya Waislamu hususan Mashia wa Nigeria".

Maandamano ya amani ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru

Mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Nigeria vinaendelea katika hali ambayo, hivi sasa nchi hiyo inakabiliwa na matatizo lukuki ya ndani na nje ya nchi. Uwepo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo na mashambulio ya huku na kule yanayoendelea kufanywa na kundi hilo yamevuruga amani na usalama ndani ya nchi na kusababisha wakaazi zaidi ya milioni mbili wa kaskazini mwa Nigeria kuyahama makaazi yao na kuwa wakimbizi. Matatizo ya kiuchumi, umasikini, ukosefu wa ajira na kukosekana usalama katika maeneo yenye utajiri wa mafuta ya kusini mwa nchi ni miongoni mwa matatizo mengine yanayoikabili Nigeria kwa sasa. Katika hali kama hiyo ambapo kurejeshwa utulivu na uthabiti wa angalau kiwango fulani linaonekana kuwa ndilo takwa muhimu zaidi la raia wa nchi hiyo,  hatua ya vikosi vya jeshi na vya usalama ya kutumia mabavu na kuwakandamiza Waislamu, yenyewe ni sababu ya kushtadi matatizo na ni kizuizi cha kupatikana umoja na uthabiti nchini Nigeria.../