Al Bashir atishia kuchukua hatua kali dhidi ya waasi Darfur
Rais wa Sudan ametishia kuchukua hatua kali dhidi ya waasi wa Darfur iwapo hawatakabidhi silaha zao.
Omar al Bashir ambaye ametumia lugha kali akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Muungano wa Kitaifa wa Vijana mjini Khartoum amesema kuwa, wale wanaomiliki silaha kinyume cha sheria watakabiliwa na adhabu kali.
Rais wa Sudan amekariri tena ahadi yake ya kung'atuka madarakani baada ya kumalizika kipindi cha uongozi wake mwaka 2010 na kwamba atakabidhi madaraka kwa amani na bila ya mapigano kwa kiongozi wa baada yake.

Takwimu zinaonesha kuwa silaha karibu milioni mbili zimezagaa baina ya raia wa Sudan na kwamba laki tatu kati ya hizo ziko katika eneo lenye machafuko la Darfur.
Machafuko ya eneo la Darfur yamesababisha vifo vya watu laki tatu na kuwalazaimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.