Maelfu waandamana Zimbabwe wakishinikiza Mugabe ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36480-maelfu_waandamana_zimbabwe_wakishinikiza_mugabe_ajiuzulu
Maelfu ya raia wameandamana leo nchini Zimbabwe hasa katika mji mkuu Harare wakiunga mkono hatua ya jeshi ya kumuondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo na kupiga nara wakishinikiza kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 ajiuzulu na kuachia madaraka ya nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2017 11:27 UTC
  • Maelfu waandamana Zimbabwe wakishinikiza Mugabe ajiuzulu

Maelfu ya raia wameandamana leo nchini Zimbabwe hasa katika mji mkuu Harare wakiunga mkono hatua ya jeshi ya kumuondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo na kupiga nara wakishinikiza kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 ajiuzulu na kuachia madaraka ya nchi.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakisema kwa sauti kubwa kwamba, 'basi inatosha," "Mugabe anapaswa kuondoka madarakani" na "Mugabe ondoka, achia uongozi."

Maandamano ya leo katika mji mkuu Harare yameongozwa na  chama tawala nchini humo cha Zanu-PF lengo likiwa ni kumshinikiza Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo ajiuzulu.

Rais Mugabe ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 37 yaani tangu nchi hiyo ijipatie uhuru amekuwa akishinikizwa kila upande ili ajiuzulu ingawa hadi sasa ameendelea kushikilia kubakia madarakani hadi muhula wake wa uongozi utakapomalizika mwakani.

Rais Robert Mugabe anayekabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu

Maji yamezidi kumfika shingoni baada ya chama chake tawala cha ZANU-PF kutaka pia ajiuzulu na kuachia uongozi wa nchi. 

Jumanne iliyopita wanajeshi wa Zimbabwe walimuondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo kama njia ya kupinga maamuzi yake ya hivi karibuni. Aidha siku hiyo hiyo Mkuu wa Jeshi la Zimbabwe, Constantino Chiwenga alimpa Rais Mugabe muda wa masaa 24 kuhakikisha amemrejesha ofisini makamu wake, Emmerson Mnangagwa, vinginevyo jeshi litangilia kati.

Jeshi la Zimbabwee lilichukua hatua hiyo baada ya Rais Mugabe kumfuta kazi makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa, wiki iliyopita, na kuashiria kuwa anapendelea mke wake Grace Mugabe, kuchukua uongozi wa chama cha Zanu-PF na kuwa Rais wa Zimbabwe baada yake.