Hali mbaya ya wahajiri wa Afrika nchini Libya
Sambamba na kuendelea hali mbaya ya wakimbizi na wahajiri wa Kiafrika nchini Libya, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameutuhumu Umoja wa Ulaya kwamba, unapuuza hali mbaya wanayokabiliwa nayo wahajiri wa Kiafrika.
Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kuashiria kwamba, hatua ya madola ya Ulaya ya kukabiliana na wahajiri wanaotoka kaskazini mwa Afrika na eneo la Mashariki ya Kati imepelekea kutokea maafa ya kusikitisha kwa wahajiri hao amesisitiza kwamba, kwa kuwa Ulaya imetiliana saini na viongozi wa Libya makubaliano ya kukabiliana na wahajiri, kwa hivyo inabeba dhima ya mgogoro uliojitokeza na inapaswa kulishughulikia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.
Matamshi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa yanatolewa katika hali ambayo, baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, akthari ya wahajiri wa Kiafrika wamekuwa wakiuzwa kama bidhaa katika masoko ya watumwa nchini Libya. Kabla ya hapo pia, Shirika la Kimataifa la Wahajiri lilikuwa limetangaza kwamba, masoko ya kuuzia watumwa yamekuwa yakifanya kazi zake katika njia wanazopitia wahajiri haramu kaskazini mwa Afrika ambapo katika masoko hayo mamia ya Waafrika wamekuwa wakiuzwa hadharani na mbele ya kadamnasi.
Mwandishi Razan Najm al-Maghribi anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Libya huru imegeuka kuwa soko kubwa la mnada ambapo haiwezekani kuionyesha sura nzuri ya nchi hiyo na hivi sasa kumekuwa kukionyeshwa taswira ya uongo na isiyo ya kweli ya Libya.
Mgogoro wa Libya na kutokuweko serikali kuu yenye mamlaka ambayo itaweza kudhibiti mipaka yake, ni mambo ambayo yameigeuza nchi hiyo kuwa kivuko cha wakimbizi na wahajiri wanaotokea Afrika wakiwa na lengo la kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri. Wahajiri hao wa Kiafrika wengi wao ni vijana, wanawake na watoto ambao kutokana na umasikini na ukosefu wa ajira na kukosekana amani na uthabiti, wamekuwa wakizikimbia nchi zao na kufanya juhudi za kuelekea barani Ulaya.
Kuenea harakati za makundi ya kigaidi na kushadidi machafuko na mizozo ya kisiasa katika akthari ya nchi za Kiafrika ni jambo ambalo limepelekea kuongezeka wimbi la wahajiri. Hayo yanajiri katika hali ambayo, baada ya nchi za Ulaya kudhibiti na kuifunga mipaka yao ili kuzuia wahajiri kutoka Mashariki ya Kati wasiingie katika nchi hizo, hivi sasa zinafanya juhudi pia za kuifunga njia ya Mediterania inayotumiwa na wahajiri wa Kiafrika.
Kuhusiana na jambo hilo ni kwa muda sasa ambapo viongozi wa Ulaya wamekuwa katika mchakato wa mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali za Kiafrika ikiwemo Niger, Mali na Libya ambapo natija ya hayo imekuwa ni kutiwa saini makubaliano ya kuzipatia fedha nchi hizo ili zitekeleze mipango ya kuwazuia wahajiri wa Kiafrika.
Katika kalibu hiyo na kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na nchi hizo na Libya ni kuwa, vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika vina jukumu la kuwazuia wahajiri wasisonge mbele zaidi ya mipaka ya Mediterania. Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Libya iko kwenye mashinikizo katika suala zima la kukabiliana na wahajiri na kuzuia taathira hasi za kiusalama, kiuchumi na kijamii.
Pamoja na kuwa kabla ya hapo pia, wahajiri wa Kiafrika walikuwa wakikabiliwa na tishio la kuzama katika Bahari ya Mediterania au hata kuangukia mikononi mwa mitandao ya biashara ya magendo ya binadamu, lakini filihali kufichuliwa wigo mpana wa kuuzwa wahajiri kama bidhaa kwa anuani ya watumwa huko Libya, kumepelekea kusikika sauti kubwa ya kengele ya hatari kuhusiana na masaibu makubwa yanayowakabili wahajiri katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Inaonekana kuwa, hatua ya madola ya Magharibi ya kutekeleza siasa mpya za kukabiliana na wahajiri imewafanya wahajiri wa Kiafrika wazidi kukabiliwa na hali mbaya. Hii ni katika hali ambayo, matatizo mengine yanayolikabili bara la Afrika bado hayajapatiwa ufumbuzi huku madola ya Magharibi yakiendelea kuwa chanzo na washadidishaji wa matatizo hayo badala ya kuwa malhamu na poza ya majeraha ya nchi za bara hilo.