Mvutano katika uhusiano wa Morocco na Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3682-mvutano_katika_uhusiano_wa_morocco_na_umoja_wa_mataifa
Baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuuelezea uwepo wa vikosi vya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi kuwa ni "ukaliaji wa mabavu", mivutano na mikwaruzano katika uhusiano wa umoja huo na Morocco imeongezeka kufikia hadi Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa, kwa wito wa serikali ya Rabat, imefunga ofisi yake ya mawasiliano ya kijeshi katika eneo la Sahara Magharibi na kuwaondoa waangalizi watatu wa kijeshi waliokuwepo katika ofisi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2016 03:17 UTC
  • Mvutano katika uhusiano wa Morocco na Umoja wa Mataifa

Baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuuelezea uwepo wa vikosi vya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi kuwa ni "ukaliaji wa mabavu", mivutano na mikwaruzano katika uhusiano wa umoja huo na Morocco imeongezeka kufikia hadi Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa, kwa wito wa serikali ya Rabat, imefunga ofisi yake ya mawasiliano ya kijeshi katika eneo la Sahara Magharibi na kuwaondoa waangalizi watatu wa kijeshi waliokuwepo katika ofisi hiyo.

Itakumbukwa kuwa siku kadhaa zilizopita, wakati alipotembelea kambi moja ya wakimbizi wa Sahara Magharibi nchini Algeria, Ban aliwaambia wakimbizi hao kuwa anaelewa fika hasira na uchungu walionao wananchi wa Sahara Magharibi kutokana na ardhi yao kuendelea kukaliwa kwa mabavu na Morocco.

Kaufuatia kauli yake hiyo, serikali ya Morocco ilimtuhumu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuwa ameshindwa kuheshimu nafasi yake ya kutakiwa kutopendelea upande wowote katika mgogoro wa Sahara Magharibi na kutishia kuwafukuza askari wote wa kulinda amani wa umoja huo walioko katika eneo hilo.

Lakini mbali na vitisho hivyo, serikali ya Morocco iliwatimua wafanyakazi 83 wa Umoja wa Mataifa waliokuwa katika eneo la Sahara Magharibi na kusitisha kulipa mchango wa dola milioni tatu za kugharamia shughuli za umoja huo katika eneo hilo.

Baraza la Usalama, likiwa ndiyo nguzo na mhimili muhimu zaidi wa Umoja wa Mataifa ambao una jukumu la kudhamini amani na usalama duniani limeshindwa kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu mvutano uliojitokeza kati umoja huo na serikali ya Morocco; na ili kujaribu kupoza na kutuliza hali ya mambo limeiacha kila nchi mwanachama ichukue msimamo wake binafsi katika kuamiliana na Rabat.

Kufuatia hatua iliyochukuliwa na Morocco, tarehe 19 mwezi huu Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa haitowezekana umoja huo kuendelea na shughuli zake nchini humo. Hata hivyo tamko hilo la Umoja wa Mataifa halikusaidia kuzima moto wa hasira za Wamorocco; kwani mamia kadhaa ya wananchi hao walifanya maandamano katika mji mkuu Rabat ya kulaani matamshi Ban Ki-moon. Waandamanaji hao walitangaza kuwa Sahara Magharibi ni sehemu ya ardhi ya Morocco na wakaituhumu harakati ya POLISARIO kuwa ina njama ya kuubadilisha muundo wa idadi ya watu wa nchi hiyo.

Eneo la Sahara Magharibi lililoko kaskazini magharibi mwa Afrika lina ukubwa wa kilomitamraba laki mbili na 26,000 na idadi ya watu wapatao laki tano ambao ni Waislamu. Tangu alipoondoka mkoloni wa Kihispania mnamo mwaka 1975 hadi sasa, eneo hilo limebaki kuwa na kitendawili cha mgogoro wa kisiasa kisichojulikana jibu lake.

Baada ya kuondoka Wahispania, harakati ya POLISARIO ilitangaza uhuru wa eneo hilo na kuliita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahara (SADR). Hata hivyo serikali ya Rabat, huku ikisisitiza kwamba Sahara Magharibi ni sehemu ya ardhi ya Morocco ililiunganisha eneo hilo na sehemu kuu ya ardhi ya nchi hiyo. Harakati ya POLISARIO, ikiungwa mkono na Algeria ikaamua kuanzisha mapambano ya kupigania uhuru na kujitawala Sahara Magharibi. Baada ya vita na mapigano ya miaka kadhaa baina ya pande mbili yaliyowafanya karibu nusu ya wakaazi wa Sahara Magharibi walihame eneo hilo, hatimaye mnamo mwaka 1991 Umoja wa Mataifa uliingilia kati kwa madhumuni ya kutafuta suluhu na ufumbuzi wa hatima ya Sahara Magharibi; na kuanzia wakati huo eneo hilo likawekwa katika hali "si ya vita, si ya suluhu".

Kuanzia mwaka huo wa 1991 askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walipelekwa Sahara Magharibi ili kusimamia Kura ya Maoni ya kuamua hatima ya eneo hilo. Kwa muda wote huo, Umoja wa Mataifa umekuwa ukiituhumu serikali ya Morocco kuwa inakiuka haki za binadamu na kuingilia kazi za askari wa kulinda wa umoja huo waliotumwa Sahara Magharibi.

Kwa msingi huo, kutumia Ban Ki-moon neno "ukaliaji wa mabavu" na kuzuka mivutano na mikwaruzano baina ya serikali ya Morocco na Umoja wa Mataifa si jambo jipya na geni; isipokuwa mivutano na mikwaruzano hiyo imeshtadi mara hii kuliko ilivyotokea katika mara zilizopita.../