Nov 27, 2017 15:03 UTC
  • Boko Haram waua wanajeshi watatu kaskazini mashariki mwa Nigeria

Duru za usalama za Nigeria zimetangaza habari ya kuuawa wanajeshi watatu katika shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la Boko Haram katika mji wa Magumeri, wa jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Duru za usalama za Nigeria zimetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, wanajeshi watatu wa serikali wameuawa katika mapigano na magaidi wa Boko Haram na wengine sita kujeruhiwa katika mji wa Magumeri. Duru hizo zimesema kuwa, magaidi wa Boko Haram waliuvamia mji huo kwa nia ya kuuteka.

 

Mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria na hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauwa kutokana na machafuko yaliyosababishwa na kundi hilo.

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya jinai za kila namna ikiwa ni pamoja na kuteka nyara watu pamoja na wasichana na kuwapiga mnada kama bidhaa. Hadi hivi sasa maelfu ya watu wametekwa nyara na kundi hilo na mamia ya maelfu ya wengine wamekimbia makazi yao kwa kuhofia mashambulizi ya genge hilo la wakufurishaji.

Kuanzia mwaka 2015 kundi hilo lilipanua mashambulizi yake na kuingia pia katika nchi jirani na Nigeria yaani Cameroon, Chad na Niger. Nchi hizo nne zimeunda jeshi la pamoja la kukabiliana na kundi hilo lakini zimeshindwa kulimaliza.

Tags