Odinga 'kujiapisha' Disemba 12, kupinga ushindi wa Kenyatta UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36955-odinga_'kujiapisha'_disemba_12_kupinga_ushindi_wa_kenyatta_un
Kinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema ataapishwa kuwa rais 'halali' wa Kenya Disemba 12, wakati nchi hiyo itakuwa inaadhimisha Siku ya Jamhuri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2017 04:52 UTC
  • Odinga 'kujiapisha' Disemba 12, kupinga ushindi wa Kenyatta UN

Kinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema ataapishwa kuwa rais 'halali' wa Kenya Disemba 12, wakati nchi hiyo itakuwa inaadhimisha Siku ya Jamhuri.

Akiwahutubia wafuasi wake hapo jana, muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, Odinga alidai kwamba alishinda kihalali uchaguzi wa Agosti 8 na hivyo muungano huo utatumia Kifungu cha Kwanza cha Katiba kumuapisha.

Amesema: "Katika uchaguzi wa Agosti 8 nilipata kura milioni 8.5 naye Uhuru akapata kura milioni 7.1. Sisi hatutambui ushindi wake katika kura ya marudio iliyofanyika Oktoba 26, Nitaapishwa kama Bw (Emmerson) Mnangagwa huko Zimbabwe…tutatumia kipengele cha kwanza cha katiba kinachowapa raia mamlaka ya juu..mimi si mwoga, sitaapishwa kienyeji kama Besigye wa Uganda."

Kenyatta akiapishwa jana Jumanne

Kadhalika amesema NASA inafanya mikakati ya kupinga ushindi wa Kenyatta katika Umoja wa Mataifa. Odinga amesema atawasilisha malalamiko rasmi kwa UN kupitia barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.

Rais Kenyatta alikula kiapo hapo jana katika Uwanja wa Kasarani mjini Nairobi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 ambao ulisusiwa na Odinga, kwa madai kuwa haukuwa huru na wa haki.

Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha uchaguzi wa Agosti 8, ikisema kuwa uligubikwa na kasoro nyingi na haukuzingatia miongozo ya sheria na katiba.