Idadi ya waliopoteza maisha katika hujuma ya kigaidi Somalia Oktoba yafika 512
(last modified Sat, 02 Dec 2017 04:15:01 GMT )
Dec 02, 2017 04:15 UTC
  • Idadi ya waliopoteza maisha katika hujuma ya kigaidi Somalia Oktoba yafika 512

Watu 512 sasa wamebainika kupoteza maisha katika miripuko miwili ya mabomu iliyojiri katika mkuu wa Somalia, Mogadishu mwezi Oktoba, imesema kamati ya kuchunguza hujuma hiyo.

Katika matukio ya kigaidi ya Oktoba 14, lori lililokuwa limesheheni mabomu liliripuka nje ya hoteli moja mashuhuri katika eneo la K5 mjini Mogadishu na masaa mawili baadaye lori jingine lililokuwa limesheni mabomu likaripuka katika eneo la Madina.

Hadi kufikia Oktoba 20, serikali ya Somalia ilikuwa imesema kuwa, idadi ya waliopoteza maisha katika miripuko hiyo miwili ilikuwa ni watu 358.

Baada ya mashambulio hayo ya kigaidi yaliyotajwa kuwa mabaya zaidi katika historia ya Somalia, serikali ya nchi hiyo iliunda kamati maalumu iliyopewa jina la Kamati ya Uokoaji ya Zobe, kwa lengo la kubaini idadi kamili ya waliopoteza maisha.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi Mogadishu

Mwenyekiti wa kamati hiyo Abdullahi Mohamed Shirwac amenukuliwa Ijumaa na vyombo vya habari akisema kuwa, hadi sasa watu 512 wamethibtishwa kupoteza maisha na wengine 316 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi.

Kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo hufanya hujuma kama hizo mara kwa mara halijatangaza kuhusika na  kwamba uchunguzi bado haujaweza kubaini mhusika.

Tags