Dec 12, 2017 08:13 UTC
  • Gaidi ajiripua na kuua watu wawili msikitini Cameroon

Mshambuliaji aliyekuwa amejifunga bomu amejiripua na kuua watu wawili katika msikiti mmoja ulioko kaskazini mwa Cameroon karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria mapema leo.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, shambulizi hilo la kujitolea muhanga limetokea alfajiri ya leo katika mji wa Kerawa, kaskazini mwa Cameroon, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria.

Mashuhuda wanasema hujuma hiyo imetokeo muda mfupi baada ya Swala ya Alfajiri, na kwamba gaidi huyo aliyetekeleza shambulio hilo ameaga dunia pia.

Septemba mwaka huu, binti wa umri wa miaka 12 aliingia katika msikiti mwingine wakati wa Swala ya Alfajiri katika kijiji cha Kolofata na kujiripua, ambapo watu watano waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Wanachama wa genge la kitakfiri la Boko Haram

Takwimu za hivi karibuni za shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International zinaonyesha kuwa, watu karibu 400 wameuawa katika mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram kuanzia mwezi Aprili mwaka huu huko Nigeria na Cameroon.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yaliyoanzia kaskazini mwa Nigeria na kusambaa hadi ndani ya ardhi za nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger yameshaua zaidi ya watu 20,000 katika eneo lote la Bonde la Ziwa Chad linalojumuisha nchi hizo nne, mbali na kuwafanya watu wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makazi.

Tags