Dec 24, 2017 07:58 UTC
  • Congo Brazaville yasaini muafaka wa amani na kundi la waasi la 'Ninja'

Serikali ya Jamhuri ya Congo imesaini makubaliano ya amani na kundi la waasi la 'Ninja' na hivyo kutamatisha mgogoro wa karibu miaka 15 ambao umesababisha makumi ya watu kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.

Katika makubaliano hayo yaliyosainiwa jana Jumamosi katika mji mkuu Brazaville, pande mbili hasimu zimekubaliana kusitisha mapigano na kuunda kamisheni ya kurejesha amani na usalama katika eneo la Pool, lililoko kusini mashariki mwa nchi, ambako waasi hao wamekuwa wakiendeshea shughuli zao.

Upande wa serikali uliwakilishwa na François Ndé, mshauri wa masuala ya usalama wa Wizara ya Mambo ya Ndani  huku upande wa waasi wa 'Ninja' wanaoongozwa na Frederic Bintsamou ambaye anafahamika kama Pastor Ntumi, ukiwakilishwa na Jean Gustave Ntondo.

Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo Brazaville

Mapigano baina ya serikali ya Congo Brazaville na kundi la Ninja ambalo linataka kushirikishwa zaidi katika serikali yaliyoanza mwaka 2002, yalishtadi Aprili mwaka 2016, baada ya Rais Denis Sassou Nguesso ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu, kushinda uchaguzi tata wa urais.

Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya upinzani katika vita vya ndani vya 1998 hadi 1999 na liliwahi kutia saini makubaliano mengine ya amani na serikali mwaka 2003.

 

Tags