Makundi ya waasi yazidi kusakamwa, wapiganaji 6 wa Mai-Mai wauawa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38245-makundi_ya_waasi_yazidi_kusakamwa_wapiganaji_6_wa_mai_mai_wauawa_drc
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuua wanachama sita wa kundi la waasi wa Mai-Mai katika eneo la Kasindi mkoani Kivu Kaskazini, siku chache baada ya wapiganaji hao kuteketeza moto nyumba ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo katika mji wa Musienene katika mkoa huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 04:20 UTC
  • Makundi ya waasi yazidi kusakamwa, wapiganaji 6 wa Mai-Mai wauawa DRC

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuua wanachama sita wa kundi la waasi wa Mai-Mai katika eneo la Kasindi mkoani Kivu Kaskazini, siku chache baada ya wapiganaji hao kuteketeza moto nyumba ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo katika mji wa Musienene katika mkoa huo.

Luteni Jules Tshikudi, msemaji wa jeshi katika eneo hilo amesema mapigano hayo yalianza saa mbili asubuhi kwa saa za nchi hiyo na kuendelea kwa masaa kadhaa, na kwamba wamepoteza askari mmoja katika makabiliano hayo.

Amesema wanajeshi watatu wa Kongo DR wamejeruhiwa pia katika tukio hilo, na kubainisha kuwa waasi watatu wa Mai-Mai wametiwa mbaroni na kwamba maafisa usalama wamefanikiwa kudhibiti hali katika eneo hilo.

Operesheni ya jana imefanyika siku moja baada ya Jeshi la Uganda UPDF kufanya mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya maficho ya kundi jingine la waasi wa ADF, katika mpaka wa nchi hiyo na Kongo DR, na kufanikiwa kuua zaidi ya 100 miongoni mwao na kujeruhi wengine wengi.

Wanachama wa genge la Mai-Mai

Disemba 25 siku ya Krismasi, jeshi la Kongo lilitangaza habari ya kuuawa askari wake 9 na wapiganaji wa Mai-Mai katika kijiji cha Lweba mkoani Kivu Kusini, wiki chache baada ya watu sita wakiwemo wanajeshi wawili kuuawa katika makabiliano mengine makali kati ya jeshi na waasi hao katika eneo la Kivu Kaskazini.

Eneo la Kivu limekuwa uwanja wa makabiliano kati ya vikosi vya usalama na magenge ya waasi, ambapo mapema mwezi huu, askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  waliuawa na 44 wengine kujeruhiwa katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini, kufuatia hujuma ya waasi wa ADF.