Burundi: Jeshi letu halijagawanyika makundi mawili
Msemaji wa jeshi la Burundi amekadhibisha habari za kugawika makundi mawili jeshi la nchi hiyo. Gaspard Baratuza ameyasema hayo kupitia mahojiano ya redio na kuongeza kuwa, ripoti za baadhi ya wanasiasa juu ya kugawika jeshi la nchi hiyo katika makundi mawili ya Kihutu na Kitutsi, hayana ukweli wowote.
Msemaji wa jeshi la Burundi pia amesema, hakuna uhusiano wowote mauaji mawili ya nyakati tofauti ya makamanda wawili wa jeshi la nchi hiyo, na kwamba kila mmoja ameuawa kwa njia tofauti.
Hayo yamekuja kufuatia mauaji ya maafisa wawili wa polisi siku ya Jumanne, katika maeneo tofauti ya Bujumbura, mji mkuu wa Burundi.
Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, uliibuka tangu mwezi Machi mwaka jana, kufuatia uamuzi wa chama tawala cha CNDD-FDD wakumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu mfululizo katika uchaguzi uliopita ambao Nkurunziza alitangazwa mshindi.