Rwanda pia yakanusha taarifa za kukubaliana na Israel kuwapokea wahajiri
Serikali ya Rwanda imekanusha taarifa za kukubali kuwapokea maelfu ya wahajiri wa Kiafrika kama sehemu ya mpango uliofikiwa baina yake na utawala wa Kizayuni wa Israel, muda mfupi baada ya Uganda kukabidhisha madai hayo ya Tel Aviv.
Waziri wa Nchi katika Masuala ya Kigeni na Ushirikiano wa Kikanda na Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe ameandika kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, nchi hiyo haijakubaliana chochote na Tel Aviv juu ya kuwapokea wahajiri wa Kiafrika kutoka Israel.
Serikali ya Kigali imekabidhisha vikali madai hayo masaa machache baada ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Uganda kuliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Kampala haijafikia makubaliano na Tel Aviv ya kupelekwa nchini humo wahajiri kutoka Israel.
Serikali ya Uganda imesisitiza kwamba, taarifa hizo ni bandia na kwamba kwa miaka minne sasa imekuwa ikikanusha juu ya kuweko mpango kama huo kati yake na Israel.
Jumatano iliyopita, Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza kutekeleza mpango wa kuwarejesha nchini kwao kwa nguvu makumi ya maelfu ya Waafrika walioingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu.
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wahajiri haramu 38,000 wa Kiafrika wana muda wa hadi mwezi Machi mwaka huu kuondoka kwa khiari, vinginevyo watakamatwa.