Jan 06, 2018 07:17 UTC
  • Mapigano mapya yaripotiwa karibu na mji mkuu wa Sudan Kusini

Mapigano mapya kati ya jeshi na waasi yameripotiwa karibu na mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, siku chache baada ya kuvurugika kwa makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya pande hasimu za kisiasa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Lul Ruai Koang, msemaji wa jeshi la nchi hiyo jana Ijumaa alisema watu kadhaa wameuawa katika makabiliano hayo mapya, yalioanza Alkhamisi usiku baada ya vikosi vya upinzani kujaribu kuiteka kambi ya jeshi iliyoko magharibi mwa Juba.

Amesema wapiganaji hao chini ya amri ya Luteni Kanali Chan Garang wameshambulia ngome ya jeshi la SPLA katika mji wa kaskazini wa Kapur, ambapo watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa.

Hata hivyo wapiganaji wanaofungamana na aliyekuwa Makamu wa Rais, Riek Machar wamekanusha vikali kuhusika na uvamizi huo dhidi ya kambi ya kijeshi.  

Rais Salva Kiir na Riek Machar

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD lililaani kitendo cha kuvunjika kwa makubaliano yaliyosainiwa na pande zinazohasimiana nchini Sudan Kusini, na kusisitiza kwamba taasisi hiyo itawachukulia hatua wanaovuruga makubaliano hayo kwa mujibu wa sheria ya kimataifa iliyopitishwa na wakuu wa nchi za jumuiya hiyo ya kieneo Novemba mwaka 2014.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

Tags