Kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38675-kuenea_mlipuko_wa_ugonjwa_wa_kipindupindu_kongo
Maafisa wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamearifu kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huko Kinshasa mji mkuu wa nchi hiyo kufuatia mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2018 04:49 UTC
  • Kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu Kongo

Maafisa wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamearifu kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huko Kinshasa mji mkuu wa nchi hiyo kufuatia mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo.

Maafisa hao wa sekta ya afya wameeleza kuwa hali ya watu walioathirika na mafuriko hayo ni mbaya huko Kinshasa na kwamba upo uwezekano wa kuenea pakubwa kpindupindu katika mji mkuu huo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mvua kubwa zilizonyesha Alhamisi iliyopita huko Kinshasa na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo zimesababisha vifo vya watu 44 na kujeruhi wengine wanne.  

Maafisa wa afya wameeleza kuwa hali ya mambo katika baadhi ya mikoa inatia wasiwasi sana kufuatia kusimamishwa kwa mpango wa kusimamia usambazaji wa maji ya kunywa. Watu 220 wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu tangu mwezi Novemba uliopita hadi sasa huku wengine 23 wakiaga dunia kwa maradhi hayo huko Kinshasa.

Wagonjwa wa kipindupindu wakiwa wamelazwa hospitali 

Umoja wa Mataifa umeashiria kuwepo hali kama hiyo katika mikoa mingine ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuutaja ugonjwa wa kipindupindu kuwa tatizo kubwa la kiafya nchini humo.