EU: Uchaguzi wa Kenya ulizungukwa na ufisadi na vitisho
Mkuu wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti na Oktoba mwaka uliomalizika 2017 nchini Kenya amesema kampeni zilizotangulia zoezi hilo ziligubikwa na rushwa, utumiaji wa mali za umma na vitisho.
Akihutubia waandishi wa habari kutoka Bunge la EU mjini Brussels hii leo, Marietje Schaake amesema rasilimali za umma zilitumika vibaya katika kampeni hizo, ambapo watu walihongwa ili kushiriki mikutano ya kampeni.
Ripoti ya timu ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya imesema baadhi ya wanasiasa nchini humo waliwatolewa vitisho maafisa wa taasisi huru na kwamba baadhi ya Wakenya hawakuwa na imani na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendesha uchaguzi huo.
Kadhalika ripoti hiyo imeashiria namna maafisa wa polisi walivyotumia nguvu kupita kiasi wakati wa harakati za kampeni na uchaguzi wenyewe na kusema kuwa 'Wakenya hawakufurahia haki yao ya kidemokrasia' katika msimu wa uchaguzi wa mwaka jana.
Mwezi uliopita, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilisema makumi ya wanawake walibakwa na maafisa wa polisi wakati wa harakati za uchaguzi mkuu huo nchini Kenya.
Kabla ya hapo, mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International yalisema polisi ya Kenya iliua watu wasiopungua 67 katika maandamano ya upinzani ya kushinikiza mabadiliko kwenye Tume ya Uchaguzi, kuelekea uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 uliosusiwa na mrengo mkuu wa upinzani NASA.