Juhudi za Ulaya kuzidisha uingiliaji wa kijeshi barani Afrika
Ikiwa ni katika mkondo wa kudumisha uingiliaji wa nchi za Magharibi barani Afrika, serikali za Italia na Uingereza zimeazimia kuimarisha uwepo wao wa kijeshi katika baadhi ya nchi za bara hilo.
Kuhusiana na suala hilo viongozi wa Uingereza wamesema kuwa wataongeza idadi ya helkopta za kijeshi za nchi hiyo kwa shabaha ya kuimarisha operesheni za jeshi la Ufaransa katika nchi ya Kiafrika ya Mali. Katika upande wa pili, bunge la Italia limepitisha mpango wa kutumwa askari 120 wa nchi hiyo huko Niger. Hatua hiyo ni katika juhudi za viongozi wa Italia za kusimamisha mkondo wa wahajiri haramu wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya kwa kisingizio cha kutafuta maisha mazuri. Hata kama nchi za Kiafrika zimekuwepo kwa miaka mingi barani Afrika kwa kisingizio cha kuimarisha amani na usalama, lakini katika miaka ya hivi karibuni nchi hizo zimeimarisha uwepo huo kwa visingizio tofauti kama vile kupambana na ugaidi na kuzuia wahajiri haramu kuelekea Ulaya.
Kuhusiana na suala la kupambana na ugaidi, hivi sasa kuna askari wengi wa nchi za Ulaya na Marekani waliotumwa barani Afrika kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. Kuongezeka kwa harakati za makundi ya kigaidi katika pembe tofauti za dunia na kushindwa vibaya kwa baadhi ya makundi hayo kama vile Daesh nchini Iraq na Syria na uwezekano wa kuhamishiwa harakati za kigaidi za kundi hilo katika nchi za Kiafrika, kumetoa kisingizio kizuri kwa nchi za Magharibi kueneza shughuli zao za kijeshi katika nchi za Kiafrika. Kubuniwa kwa kundi la Sahel 5 kwa madai ya kupambana na ugaidi katika eneo hilo, ni hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na nchi za Magharibi zikiongozwa na Ufaransa. Kwa kuunda kundi hilo la pamoja la kijeshi, Ufaransa ina lengo la kuimarisha uwepo wake wa kijeshi barani Afrika na wakati huohuo kugawana gharama za kijeshi za operesheni za kundi hilo na nchi nyingine za Magharibi, kama ambavyo tayari imekwishapata uungaji mkono na ahadi za kuimarisha shughuli za kundi hilo kutoka kwa washirika wake kadhaa wa Magharibi. Katika upande mwingine, Marekani tayari imeongeza idadi ya askari wake barani Afrika kwa kisingizio hichohicho eti cha kupamaba na ugaidi.
Uwepo wa kijeshi wa nchi za Ulaya na Marekani barani Afrika si tu kwamba haujakuwa na faida yoyote kwa bara hilo bali bali umakuwa na madhara makubwa kwa Waafrika kwa kufanya nchi zao kuwa uwanja wa mashindano ya kijeshi na kiuchumi ya madola makubwa ya Magharibi. Ni kwa msingi huo ndipo wataalamu wengi wa masuala ya kijeshi na kisiasa wakasema kuwa nchi za Magharibi hazipasi kupewa fursa ya kujiimarisha katika nchi za Kiafrika kwa sababu madola hayo ya kigeni na hasa Marekani, yanafuatilia tu maslahi yao ya kiuchumi na kudhibiti masoko ya Afrika kwa manufaa yao binafsi.
Kudhibitiwa wahajiri haramu wanaoelekea nchi za Ulaya ni kisingizio kingine kinachotumiwa na nchi za Magharibi kueneza satwa na uwepo wao katika nchi za Kiafrika. Msaada wa kifedha wa Italia kwa Niger pia umetolewa kwa lengo la kusimamisha mkondo wa maelfu ya wahajiri wa nchi hiyo wanaovuka mpaka na kuingia Libya kwa madhumuni ya kuendelea na safari yao kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Kwa vyovyote vile ukweli wa mambo ni kuwa kabla ya kuwa nchi za Ulaya na Marekani zinafuatilia suala la kupambana na ugaidi, zinataka kujiimarisha barani Afrika kwa shabaha ya kuwa na nafasi nzuri ya kushindana kiuchumi na kudhibiti maeneo ya kistratijia ya bara hilo muhimu.