Makumi ya watoto waokolewa kutoka shule ya al-Shabaab Somalia
Serikali ya Somalia imesema askari wa nchi hiyo wamevamia shule iliyokuwa ikiendeshwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab na kuokoa makumi ya watoto toka kwenye makucha ya genge hilo la ukufurishaji.
Abdirahman Omar Osman, Waziri wa Habari wa Serikali ya Federali ya Somalia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, watoto 32 walionusuriwa usiku wa kuamkia leo wamekuwa wakipokea mafunzo ya kuwa na misimamo mikali ya kufurutu ada katika shule hiyo inayoendeshwa na wanamgambo wa al-Shabaab.
Amesema kitendo hicho cha kuwateka nyara na kuwapa mafunzo kwa nguvu watoto wadogo kinaonyesha ni jinsi gani kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limepoteza ushawishi na linaelekea kusambaratika.
Hata hivyo msemaji wa al-Shabaab, Abdiasis Abu Musab anadai kuwa wanajeshi wa serikali wakisaidiwa na ndege zisizo na rubani wameshambulia shule hiyo iliyoko katika eneo la Middle Shabelle, na kuua wanafunzi wanne na mwalimu mmoja.
Hivi karibuni, ripoti iliyotolewa na ofisi ya Human Rights Watch (HRW) mjini Nairobi ilisema kuwa, shirika hilo limezungumza na Wasomali ambao wanalalamika kwamba wanamgambo wa al-Shabaab katika miezi ya hivi karibuni wamewateka watoto wao, wavulana na wasichana, na kuwalazimisha wajiunge la kundi kundi hilo kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi.
Ripoti ya Human Rights Watch imesema maelfu ya watoto wamesajiliwa kama wapiganaji wa mstari wa mbele na kwamba mamia ya wengine wamelazimika kukimbia makazi na nyumba zao kwa kuhofia kulazimishwa kujiunga na kundi la al Shabab.