Jeshi la Somalia laukomboa mji uliokuwa ukishikiliwa na Al Shabab
(last modified Sat, 20 Jan 2018 04:38:58 GMT )
Jan 20, 2018 04:38 UTC
  • Jeshi la Somalia laukomboa mji uliokuwa ukishikiliwa na Al Shabab

Jeshi la Somalia limeukomboa mji wa kusini wa Bar-Sanguni uliokuwa ukishikiliwa na kundia la magaidi wakufurishaji wa Al-Shabaab, na kuwaua wapiganaji saba wa kundi hilo, wakiwemo makamanda wake wanne waandamizi.

Kamanda mkuu wa divisheni ya 43 ya jeshi la Somalia iliyoshiriki kwenye operesheni hiyo Jenerali Ismail Sahardid hakutaja idadi ya majeruhi kwa jeshi lake kwenye operesheni hiyo, na kuongeza kuwa jeshi lake limewakamata mafundi wawili waliokuwa wakihudumu katika kundi hilo la kigaidi.

Jeshi la Somalia limeimarisha operesheni zake za angani na nchi kavu dhidi ya Al Shabaab, kufuatia kuanza hatua kwa hatua mchakato wa kuondoka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini humo maarufu kama AMISOM.

Kikosi cha majeshi ya Umoja wa Afrika cha AMISOM ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007. 

Kikosi hicho kinaundwa na askari elfu 22 kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopia.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Magaidi wa al Shabab wamezidisha mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu katika wiki za hivi karibuni hususan katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. 

Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliripoti kuwa kundi la kigaidi la al Shabab nchini Somalia linawalazimisha wananchi kuwakabidhi watoto wao kwa kundi hilo.

Ripoti hiyo imesema tangu mwezi Septemba mwaka jana kundi la al Shabab limekuwa likiwataka wazee, walimu wa shule za kidini na jamii za maeneo ya vijijini kukabidhi watoto wao wenye umri wa kuanzia miaka 8 la sivyo watakabiliwa na mashambulizi. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa kundi hilo lilianza kusajili watoto hao katikati ya mwaka 2017. 

Tags