Wanigeria waendeleza maandamano ya kutaka Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39213-wanigeria_waendeleza_maandamano_ya_kutaka_sheikh_ibrahim_zakzaky_aachiliwe_huru
Wananchi wa Nigeria Ijumaa waliendeleza maandamano ya kutaka serikali ya nchi hiyo imuachilie Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 20, 2018 03:37 UTC
  • Wanigeria waendeleza maandamano ya kutaka Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru

Wananchi wa Nigeria Ijumaa waliendeleza maandamano ya kutaka serikali ya nchi hiyo imuachilie Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu, Abuja ambapo, washiriki walisisitiza kuwa Sheikh Zakzaky anashikiliwa kinyume cha sheria na hivyo wameitaka serikali imuachilie mara moja na bila masharti.

Maandamano hayo yaliyofanyika nje ya Msikiti wa Kitaifa wa Abuja yaliandaliwa na mashirika ya kiraia na ya kutetea haki za binadamu kwa lengo la kuishinikiza serikali imuachilie huru Sheikh Zakzaky.

Jumamosi iliyopita, Sheikh Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye kwa miaka miwili sasa anashikiliwa kinyume cha sheria, kwa mara ya kwanza alionekana hadharani akihojiwa na waandishi habari. Wakuu wa Nigeria walimruhusu Sheikh Zakzaky aonekane hadahrani baada ya kuenea uvumi kuwa amepoteza maisha akiwa kizuizini.

Maandamano ya wananchi wa Nigeria wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inasisitiza kuwa serikali lazima itekeleze amri ya mahakama ya kumuachilia huru badala ya kujihusisha na sarakasi za kueneza klipu za video.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.

Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo ambalo limenyamaziwa kimya na Umoja wa Mataifa.