Jeshi la Kongo DR latangaza vita dhidi ya makundi mawili yanayobeba silaha
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kuwa jeshi limeingia vitani kupambana na makundi mawili yanayobeba silaha ili kukabiliana na machafuko na kukosekana kwa amani mashariki mwa nchi hiyo.
Crispin Atama Tabe amesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinapambana kwa wakati mmoja na kundi la waasi wa Uganda la ADF katika mkoa wa Kivu Kaskazini na kundi wanamgambo wanaobeba silaha la Yakutumba katika mkoa wa Kivu Kusini.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Kongo DR mapigano makali yamejiri kati ya vikosi vya jeshi na wapiganaji wa makundi hayo mawili ya waasi.
Hata hivyo Atama Tabe amekataa kueleza chochote kuhusu hasara zilizopata pande husika katika mapigano hayo.
Tangu miaka ishirini iliyopita kundi la waasi wa Uganda la ADF limekuwa likiendesha harakati zake katika maeneo kadhaa ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mbali na kundi hilo, makundi mengine kadhaa ya wanamgambo likiwemo la Mai Mai yanaendesha harakati zao kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo.
Licha ya kuwepo askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kongo DR hususan mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yangali yanaendelea kushuhudia machafuko na kukabiliwa na hatari za mashambulio ya wanamgambo na waasi wa Uganda.
Ripoti zinaeleza kuwa tangu mwezi Oktoba mwaka 2014 hadi sasa, maelfu ya watu wakiwemo makumi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika mapigano na machafuko yaliyotokea kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.../