Papa asikitishwa na mauaji ya waandamanaji Kongo DR
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa mwito wa kukomeshwa mauaji na ukandamizaji unaofanywa na maafisa usalama dhidi ya waandamanaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akihutubia umati uliojitokeza katika Medani ya St. Peter’s mjini Vatican hii leo, Papa Francis ameeleza kusikitishwa kwake na habari za kutia wasi wasi kutoka Kongo DR, ambapo watu kadhaa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga utawala wa Rais Joseph Kabila.
Amezitaka pande husika kutumia njia za amani kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo. Ifahamike kuwa, viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kongo ndio walioshinikiza kufanyika maandamano dhidi ya Kabila hivi karibuni.
Uamuzi wa Rais Joseph Kabila wa kukataa kung'atuka madarakani baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika Desemba 2016 umechochea maandamano kadhaa ya upinzani na kusababisha makumi ya watu kuuawa mbali na kushajiisha uasi wa makundi yanayobeba silaha katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Jumapili iliyopita, watu wasiopungua sita waliuawa katika maandamano ya kumtaka Kabila aachie ngazi katika mji mkuu Kinshasa.
Msemaji wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema kuwa, watu 68 wamejeruhiwa na 121 wametiwa nguvuni na kwamba Umoja wa Mataifa una habari kuhusu idadi ya watu wengine waliouawa katika maandamano yaliyofanyika katika maeneo mengine ya Kongo.