Raia elfu 7 wa Kongo wakimbilia Burundi ndani ya siku tatu
Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekimbilia nchi jirani ya Burundi kwenda kutafuta hifadhi katika kipindi cha siku tatu zilizopita.
Polisi ya Burundi imesema toka siku ya Jumatano hadi jana Ijumaa, imerekodi wakimbizi 6,692 raia wa Kongo, wanaokimbia mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa Yakutumba, katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kusini.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, mamia ya boti za kila aina zilizobeba Wakongomani zimeonekana zikivuka Ziwa Tanganyika kuelekea Burundi.
Mwezi uliopita, Sirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilitangaza habari ya raia 4500 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukimbilia Uganda katika kipindi cha siku kadhaa za mwezi huo.
Kadhalika raia zaidi ya elfu tisa wa Kongo walioathiriwa na vita mwezi Aprili mwaka jana walikimbilia nchi jirani ya Angola kwa ajili ya kutafuta hifadhi.
Usalama umekuwa ukizirota kote DRC tokea Disemba mwaka 2016 wakati Rais Joseph Kabila alipokataa kuachia ngazi pamoja na kuwa muhula wake ulikuwa umemalizika kikatiba.