Umoja wa Afrika kuwawekea vikwazo wanaohatarisha amani Sudan Kusini
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema umoja huo utawawekea vikwazo wale wote wanakwaza na kutatiza juhudi za kurejesha amani na usalama nchini Sudan Kusini.
Moussa Faki ambaye alikuwa akizungumza jana katika mkutano wa viongozi wa Afrika unaofanyika nchini Ethiopia amelaani ukatili na unyama wa kiendawazimu unaofanywa na makundi hasimu huko Sudan Kusini ambao hadi sasa umeua makumi ya maelfu ya raia wasio na hatia.
Mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika ulianza jana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ukijadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mizozo na changamoto kuu zinazozikabili baadhi ya nchi za Afrika, ugaidi, na suala la kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambaye pia anahudhuria mkutano huo amesema umoja huo utaunga mkono mpango wowote wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya kupambana na watu au makundi yanayovuruga amani huko Sudan Kusini.
Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 miaka miwili tu baada ya kujitenga na jamhuri ya Sudan.