Watu 9 wauwa katika mapigano Kasai, Kongo DR
Kwa akali watu tisa wameripotiwa kuuawa katika mapigano ya siku mbili katika eneo la Kasai, huko Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.
Jacopo Pembe Longo, afisa wa serikali katika mkoa wa Kasai amewaambia waandishi wa habari kuwa, wapiganaji wa kundi la waasi wa Kamwina Nsapu wameua watu wanne katika kijiji cha Bata Ishama, mkoani Kasai jana Jumatatu.
Ameongeza kuwa, waasi hao ambao walikuwa wamevalia vitambaa vyekundu vichwani huku wakiwa wamejizatiti kwa bunduki na mapanga leo Jumanne wameua watu watano katika kijiji cha Kakenge, umbali wa kilomita 12 toka kijiji walichovamia jana na kuua.
Kiongozi wa kidini katika eneo hilo, Kasisi Wilfrid Imboyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mbali na kutekeleza mauaji hayo, waasi hao wameteketeza moto zaidi ya nyumba 30 na hospitali moja katika mkoa wa Kasai.
Mkoa wa Kasai umekuwa uwanja wa makabiliano kati ya jeshi la serikali na waasi wa Kamwina Nsapu, kiongozi wa kikabila aliyeuawa na maafisa usalama mnamo Septemba mwaka 2016. Kundi la Kamwina Nsapu lilianzisha harakati hizo kupinga hatua ya Rais Joseph Kabila kuendelea kung'ang'ania madaraka licha ya muhula wake kisheria kumalizika.
Zaidi ya watu elfu tatu wameuawa huku wengine zaidi ya milioni moja na laki nne wakipoteza makazi yao tokeo wakati huo katika eneo hilo.