AU,EU wamkosoa kinara wa upinzani Kenya, Odinga, kwa kujiapisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39843-au_eu_wamkosoa_kinara_wa_upinzani_kenya_odinga_kwa_kujiapisha
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini KenYa, Raila Odinga amelaaniwa vikali na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika kwa kujiapisha kama 'rais wa wananchi' Januari 30 na kusema hatua hiyo inakiuka utawala wa sheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2018 01:20 UTC
  • AU,EU wamkosoa kinara wa upinzani Kenya, Odinga, kwa kujiapisha

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini KenYa, Raila Odinga amelaaniwa vikali na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika kwa kujiapisha kama 'rais wa wananchi' Januari 30 na kusema hatua hiyo inakiuka utawala wa sheria.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema anafuatilia kwa karibu hali ya kisiasa nchini Kenya.

Amekumbusha kuwa timu ya Umoja wa Afrika ya waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Kenya iliongozwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na kwamba uchaguzi huo ulishaidhinishwa na mahakama ya kilele nchini Kenya. Amesema Umoja wa Afrika  unapinga vikali vitendo vyote vinavyovuruga utaratibu wa katiba na utawala wa sheria. Ametoa wito kwa wapinzani Kenya kujiepusha na vitendo ambavyo vitavuruga uthabiti katika nchi hiyo.

Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga, aliyejiapisha kama 'rais wa wananchi'

Umoja wa Ulaya pia katika taarifa umesema kuheshimu sheria nchini Kenya kunajumuisha pia kumtambua Uhuru Kenyatta kama Rais wa Kenya. Katika taarifa EU imesema uchaguzi umemalizika nchini Kenya na kwamba changamoto zilizoibuka kuhusu mchakato wa uchaguzi zinapaswa kushughulikiwa.

Odinga anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi uliofanyika Agosti nane mwaka uliopita, uchaguzi ambao ulibatilishwa na mahakama iliyaomuru uchaguzi wa marudio ufanyike. Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26 ambao Odinga aliusisia.