Watu watatu wauawa, 6 wajeruhiwa kaskazini mwa Misri
Duru za Misri zimetangaza kuwa, watu watatu wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa katika tukio la karibuni kabisa la kushambuliwa polisi wa Misri, kusini mwa al Arish, makao makuu ya jimbo la Sinai Kaskazini, nchini Misri.
Mtandao wa habari wa al Akhbarul al Yaum wa nchini Misri umezinukuu duru za usalama za nchi hiyo zikisema kuwa, mtu mmoja kati ya waliouwa na mwengine mmoja kati ya waliojeruhiwa walikuwa ni raia wa kawaida.
Vile vile duru za usalama za Misri zimetangaza kuwa, makumi ya polisi na maafisa usalama wa nchi hiyo wameshauwa tangu mwaka 2011 hadi hivi sasa.
Machafuko na mauaji nchini Misri yameongezeka tangu mwaka 2013 baada ya Jenerali Abdul Fattah el Sisi ambaye ni rais wa hivi sasa wa nchi hiyo, kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani Mohammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo.
Magenge ya kigaidi yenye misimamo mikali yameigeuza Rasi ya Sinai ya kaskazini mwa Misri kuwa kituo chao kikuu cha kufanyia mashambulizi mbalimbali nchini humo kiasi kwamba idadi kubwa ya wanajeshi na maafisa wa serikali wameuawa katika eneo hilo.
Tarehe 28 Disemba mwaka jana, wanajeshi sita wa Misri waliuawa katika shambulizi la bomu lililotokea katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi hiyo. Katika tukio hilo, bomu la kutegwa ardhini liliripuka baada ya kukanywagwa na gari la jeshi lililokuwa likilinda doria katika mji wa Bir al-Abd, kaskazini mwa Rasi ya Sinai.