Wafanyakazi wawili wa kutoa misaada wauawa DRC
Wafanyakazi wa shirika moja la Ufaransa la kutoa misaada wameuawa katika mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku wa tatu akichukuliwa mateka.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema watatu hao ambao wote ni raia wa DRC walikuwa wakifanya kazi na shirika la kutoa misaada la Hydraulique Sans Frontieres.
Hujuma hiyo ilijiri katika kijiji cha Mushikiri katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Ingawa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo, wanamgambo wa Mai Mai wanaendesha uasi katika eneo hilo na maafisa wa usalama wanasema kuna uwezekano kwamba ndio waliofanya hujuma hiyo.

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu uvunjivu wa amani na usalama katika mkoa wa Kivu Kaskazini na kusema hali hiyo inavuruga shughuli za utoaji misaada kwa maelefu ya wahitaji katika eneo hilo.
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, makundi mbalimbali ya waasi na wanamgambo yamekuwa yakiendesha shughuli zao katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.