Twaweza: Masikini wanazidi kuwa masikini na matajiri kuwa matajiri zaidi Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41007-twaweza_masikini_wanazidi_kuwa_masikini_na_matajiri_kuwa_matajiri_zaidi_kenya
Uchunguzi umeonyesha kwamba, maskini wamezidi kuwa maskini huku wale wenye uwezo wa kifedha wakiendelea kuwa matajiri zaidi nchini Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2018 01:21 UTC
  • Twaweza: Masikini wanazidi kuwa masikini na matajiri kuwa matajiri zaidi Kenya

Uchunguzi umeonyesha kwamba, maskini wamezidi kuwa maskini huku wale wenye uwezo wa kifedha wakiendelea kuwa matajiri zaidi nchini Kenya.

Hayo yameelezwa kupitia utafiti uliofanywa na shirika la kijamii la Twaweza mwaka jana nchini Kenya. Utafiti huo uliofanywa kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka jana 2017 umeonyesha kuwa asilimia kubwa ya wananchi hawakuwa na uwezo wa kifedha wa kujikimu kutokana na ughali wa maisha huku matajiri wakizidi kujiimarisha kwa utajiri wao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni mtu mmoja tu kati ya watatu aliyekuwa na uwezo wa kujikimu kimaisha.

Victor Rateng, afisa mkuu msimamizi wa programu katika Shirika la Twaweza

Victor Rateng, afisa mkuu msimamizi wa programu katika Shirika la Twaweza ambalo limepata umashuhuri hivi karibuni kutokana na tafiti zake mbalimbali zikiwemo zilizofanyika Tanzania amesema kuwa, ukuaji ulishuhudiwa katika maeneo ya mijini na mashambani kati ya matajiri na maskini. Aidha ameongeza kwamba, gharama kubwa ya maisha na mfumko wa bei wa bidhaa uliorodheshwa kama suala kuu lililoathiri sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya wananchi nchini humo. Hata hivyo amekiri juu ya suala la kupungua kwa hali ya mfumuko wa bei ndani ya taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka jana ingawa amesema kuwa, punguzo hilo bado lilikuwa ni changamoto kuu kwa wananchi.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya

Kadhalika ameonyesha matarajio kwamba hali ya mambo itaboreka kidogo iwapo serikali itatekeleza mradi wa kuzalisha unga wenye bei nafuu. Aidha katika utafiti huo, asilimia 21 ya wananchi, walieleza hofu ya kisiasa kuwa ilikuwa changamoto kubwa, huku suala la njaa na ukame likiorodheshwa katika nafasi ya tatu kati ya masuala makuu yaliyowaathiri pakubwa wananchi wakati wa utafiti huo. Pia, ulieleza kuwa asilimia 82 ya wananchi hawakupendezwa na mwelekeo wa taifa kiuchumi. Kadhalika Bwana Victor Rateng, ametahadharisha kwamba huenda hali ya kiuchumi ikazorota zaidi nchini humo hasa kutokana na deni kubwa la serikali kutokana na mikopo inayochukua.