Umoja wa Mataifa wasisitiza udharura wa kudhaminiwa amani DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41019-umoja_wa_mataifa_wasisitiza_udharura_wa_kudhaminiwa_amani_drc
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu amesisitiza juu ya azma ya umoja huo ya kudhamini amani na usalama pamoja na kutekelezwa makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2018 04:16 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasisitiza udharura wa kudhaminiwa amani DRC

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu amesisitiza juu ya azma ya umoja huo ya kudhamini amani na usalama pamoja na kutekelezwa makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama katika eneo hilo.

Said Djinnit ambaye ni mwanadiplomasia wa Kialgeria amesema hayo mjini Addis Ababa Ethiopia katika kikao cha kujadili mwenendo wa utekelezwaji wa makubaliano hayo ambapo wajumbe wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa walishiriki katika mkutano huo.

Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu amesisitiza katika kikao hicho kwamba, umoja huo unafanya kila uwezalo ili kuhakikisha kwamba, makubaliano hayo yanatekelezwa na hivyo kudhamini amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu hususan katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Said Djinnit, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu

 

Makubalino hayo yalitiwa saini Februari mwaka 2013 na nchi 11 za Kiafrika na lengo lilikuwa ni kuchunguza sababu zinazoibua machafuko na ukosefu wa amani na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na eneo zima la Maziwa Makuu.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, kuna wakimbizi milioni 11 katika eneo la Maziwa Makuuu Afrika ambapo milioni tano kati yao wamekimbilia katika nchi za jirani na idadi iliyobakia ni wakimbizi wa ndani ya nchi zao.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inashuhudia machafuko katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ambapo makumi ya watu wameuawa huku mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ukiendelea kushuhudiwa.