Rais wa Kenya na kiongozi wa upinzani waahidi kukomesha migawanyiko + Sauti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41429-rais_wa_kenya_na_kiongozi_wa_upinzani_waahidi_kukomesha_migawanyiko_sauti
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo asubuhi alifanya mkutano wa kushtukiza na hasimu wake wa kisiasa ambaye pia ni kinara wa muungano wa upinzani nchini humo NASA katika jumba la Harambee jijini Nairobi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 09, 2018 13:01 UTC

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo asubuhi alifanya mkutano wa kushtukiza na hasimu wake wa kisiasa ambaye pia ni kinara wa muungano wa upinzani nchini humo NASA katika jumba la Harambee jijini Nairobi.

Mkutano huo ni wa kwanza kufanywa na viongozi hao wawili ana kwa ana tangu wahitilafiane kufuatia uchaguzi wa rais wa tarehe 8 mwezi Agosti mwaka jana uliokuwa na ushindani mkali na uchaguzi wa marudio wa tarehe 26 Oktoba ambao ulisusiwa na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mazungumzo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga (kulia pichani) 

Ajenda kuu ya mazungumzo yao ilikuwa kutafuta njia za kuungana na kuhuisha Kenya baada ya uchaguzi huo wa rais wa mwaka jana.

Katika mkutano wao wa leo, Rais Uhuru Kenyatta na Bwana Raila Odinga wameahidi kuwaunganisha Wakenya baada ya chaguzi za mwaka jana ambapo watu wasiopungua 100 waliuawa katika ghasia zilizotokea kati ya wafuasi wa upinzani na askari usalama.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa, kufanyika mkutano huo wa kushtukiza huwenda kukapelekea kupungua hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Kenya. Akizungumza mapema leo katika mkutano huo kupitia matangazo yaliyorushwa hewani moja kwa moja kwa njia ya televisheni, Odinga amesema kuwa, wakati umewadia wa kutatua hitilafu kati yao.

Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa wao wakiwa kama viongozi wana wajibu wa kutatufa suluhisho la matatizo yaliyopo kuanzia malalamiko ya uchaguzi hadi hali ya mivutano baina ya makundi ya kikabila na suala la ufisadi.