UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakazi wa mashariki mwa Congo DR
Taasisi za Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa, wakazi wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hususan katika mkoa wa Ituri wanakabiliwa na hali mbaya.
Taasisi hizo zimeashiria mgogoro mkubwa na hali mbaya inaoongezeka kila uchao katika mkoa huo na kutangaza kuwa, tangu mwezi Disemba mwaka jana zaidi ya watu 120 wameuawa katika eneo hilo na wengine elfu mbili wamechomwa moto.
Taasisi hizo za Umoja wa Mataifa zimesisitiza kuwa, wanawake na watoto wadogo ndio walengwa nambari moja wa ubakaji na ukatili wa wapiganaji wa makundi ya waasi.
Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa, hadi sasa zaidi ya watu laki tatu wamekimbia makazi yao katika mkoa wa Ituri kutokana na machafuko na ukosefu wa amani. Ripoti hiyo inasema kuwa, idadi ya wakimbizi inaongezeka kila siku katika eneo hilo hasa kwa kuzingtia kwamba, ni vigumu kufika katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na machafuko.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetadharisha kuwa, zaidi ya watoto milioni mbili wanakabiliwa na hatari ya kifo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iwapo hawatapewa misaada ya kibinadamu. Watoto laki tatu kati yao wako katika mkoa wa Kasai ulioko katikati mwa nchi hiyo.