Ghasia na machafuko yashadidi kaskazini mashariki mwa Congo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41529-ghasia_na_machafuko_yashadidi_kaskazini_mashariki_mwa_congo_dr
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kushadidi kwa ghasia na machafuko huko kaskazini mashariki kwa nchi hiyo kumewatia wasiwasi mkubwa wakazi wa maeneo hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2018 23:39 UTC
  • Ghasia na machafuko yashadidi kaskazini mashariki mwa Congo DR

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kushadidi kwa ghasia na machafuko huko kaskazini mashariki kwa nchi hiyo kumewatia wasiwasi mkubwa wakazi wa maeneo hayo.

Henri Mova ameashiria machafuko na ukatili mkubwa unaofanyika katika mkoa wa Ituri huko kaskazini mashariki mwa Congo DR na kusema kuwa, wakazi wengi wa maeneo hayo wana wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko hayo. 

Henri Mova ameongeza kuwa, makundi ya waasi yanayoshambulia raia katika mkoa wa Ituri yanachoma moto nyumba na mashamba yao. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, ameanza mashauriano na maafisa, watu mashuhuri, wawakilishi wa jumuiya za kiraia na wakuu wa makabila ya mkoa wa Ituri ili kutafuta suluhisho la hali hiyo. Ameongeza kuwa kesi ya kushughulikia mafaili ya watu 53 wanaotuhumiwa kuhusika na ukatili wa sasa katika mkoa huo itaanza wiki ijayo. 

Watoto na wanawake, waathirika wakuu wa machafuko ya Congo DR

Siku chache zilizopita pia taasisi za Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa, wakazi wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hususan katika mkoa wa Ituri wanakabiliwa na hali mbaya. 

Taasisi hizo zimesisitiza kuwa mamia ya watu wameuawa katika ghasia na machafuko yanayoendelea katika maeneo hayo hususan katika mkoa wa Ituri. 

Taasisi hizo za Umoja wa Mataifa zimesema kuwa, wanawake na watoto wadogo ndio walengwa nambari moja wa ubakaji na ukatili wa wapiganaji wa makundi ya waasi.