Zerrougui: Changamoto nyingi zinaikabili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na changamoto na matatizo mengi kuhusu suala la kuendesha uchaguzi mwaka huu wa 2018.
Bi Leila Zerrougui amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa viongozi wa Kongo wanapasa kuyapatia ufumbuzi masuala muhimu mengi yanayohusiana na mchakato wa uchaguzi ili kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi wa rais, bunge na wa serikali za mitaa mwezi Disemba mwaka huu.
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Kongo amesisitiza kuwa viongozi wa Kinshasa wanapasa kuridhiwa katika nyanja zote na khususan katika suala la uchaguzi na wale wote waliosaini muafaka wa kisiasa nchini humo. Bi Zerrougui ameongeza kuwa kugawana maeneo ya uwakilishi bungeni, kudhamini vyanzo vya fedha vinavyohitajika kuendeshea uchaguzi pamoja na hitilafu zilizopo kuhusu utumiaji wa mashine za kupigia kura ni miongoni mwa matatizo ya kimsingi ambayo viongozi wa Kinshasa wanapasa kuyapatia ufumbuzi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetumbukia katika mgogoro wa kisiasa kufuatia kuakhrishwa mara kadhaa uchaguzi wa rais na kuendelea kusalia madarakani Rais Joseph Kabila licha ya muhula wake kumalizika. Muhula wa kisheria wa kusalia madarakani Rais Kabila ilikuwa ni hadi tarehe 20 Disemba mwaka 2016.