Mar 13, 2018 17:21 UTC
  • Wataalamu wa UN: Facebook imechangia mauaji ya Waislamu wa Rohingya

Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameulaumu mtandao wa kijamii wa Facebook kwa kuruhusu uchochezi wa machafuko na ukatili dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari huko Myanmar wamesema kuwa, mtandao wa kijamii wa Facebook umekuwa na nafasi kubwa katika ukatili unaofanywa na Mabudha wa Myanmar dhidi ya jamii ya Rohingya kwa kuruhusu uenezaji wa maneno ya chuki.

Vilevile Mkaguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Yanghee Lee amesema kuwa Facebook imekuwa sehemu kubwa ya maisha ya umma, ya kiraia na ya kibinafsi nchini Myanmar na serikali imetumia mtandao huo wa kijamii kueneza habari kwa umma. Lee ameongeza kuwa, chombo hicho kimetumiwa kueneza chuki baina ya raia dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Lee: Facebook imekuwa dudu kwa Waislamu wa Rohungya

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, mtandao wa kijamii wa Facebook unatumiwa na Mabudha wenye misimamo mikali kueneza na kuchochea ukatili na chuki dhidi ya watu wa jamii ya Rohingya na jamii nyingine za waliowachache. Amesisitiza kuwa ana hofu kwamba, sasa Facebook imegeuka na kuwa dudu, kinyume kabisa na malengo yake ya asili. 

Makundi ya Wabudha wanaoungwa mkono na vikosi vya jeshi la Myanmar vimeanzisha kampeni ya mauaji dhidi ya familia za Waislamu wanaoishi katika jimbo la Rakhine. Maelfu ya Waislamu hao wameuawa, wanawake na wasichana wamebakwa na malaki ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Tags