Mahakama ya Juu Uganda yatupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4171-mahakama_ya_juu_uganda_yatupilia_mbali_kesi_ya_kupinga_ushindi_wa_museveni
Mahakama ya Juu ya Uganda imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Waziri Mkuu wa zamani nchini humo Amama Mbabazi ya kupinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa rais wa Februari mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2016 09:33 UTC
  • Mahakama ya Juu Uganda yatupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Museveni

Mahakama ya Juu ya Uganda imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Waziri Mkuu wa zamani nchini humo Amama Mbabazi ya kupinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa rais wa Februari mwaka huu.

Akisoma uamuzi huo hii leo, Jaji Mkuu Bart Katureebe amesema kuwa Mbabazi ameshindwa kutoa ushahidi unaoonyesha kuwa Rais Museveni aliwahonga wapiga kura na kwamba sehemu kubwa ya ushahidi uliotolewa mahakamami hapo ulizungukwa na kauli za uvumi sizizo na msingi.

Kadhalika Mahakama ya Juu ya Uganda imesema Mbabazi ameshindwa kutoa ushahidi unaoonyesha kuwa Rais Museveni aliwatishia maisha wapiga kura katika baadhi ya maneo na haswa ngome za upinzani na kuwalazimisha wampigie kura. Aidha Jaji Kutureebe amesema hakuna msingi madhubuti wa kuhesabiwa tena kura katika wilaya 44 kama alivyotaka Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda, kwa madai kuwa kulikuwa na uchakachuaji wa matokeo huku akisisitiza kuwa Rais Museveni alishinda kihalali katika uchaguzi huo.

Hii ni katika hali ambayo, kinara wa upinzani nchini humo Dakta Kizza Besigye amesema hakuna mchakato wowote unaoweza kuhalalisha ushindi wa Rais Museveni katika uchaguzi huo wa Febrauari 18. Besigye, mkuu wa chama cha FDC na ambaye kwa sasa yuko katika kifungo cha nyumbani tangu baada ya uchaguzi huo amesema kuwa: “Huwezi kumzuilia hasimu wako wa kisiasa iwapo una uhakika kuwa ulishinda uchaguzi kihalali.”

Februari 20, Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilimtangaza Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa kiti cha rais kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 18 mwezi huo, kwa kupata asilimia 61 ya kura zote sahihi zilizopigwa.