Mahakama: Rais Zuma alikiuka katiba, arejeshe fedha zilizofujwa
Mahakama ya Juu ya Afrika Kusini imemuagiza Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo kuirejeshea serikali sehemu ya dola milioni 16 za Marekani zilizotumika kukarabati makazi yake binafsi, kwenye moja ya kashfa kubwa za ufisadi zilizowahi kuripotiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Jopo la majaji 11 wa mahakama hiyo ya katiba limesema kuwa Rais Zuma alikiuka miongozo ya katiba kwa kukataa kutii maagizo ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kuhusiana na uchunguzi wa sakata hilo. Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mogoeng Mogoeng ameipa Wizara ya Fedha ya nchi siku 60 kuamua ni kiasi gani Zuma atairejeshea serikali na baada ya hapo Rais huyo atakuwa na siku 45 kulipa fedha hizo. Mogoeng amesema ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Umma ni moja ya taasisi ambazo zimekuwa katika mstari wa mbele kupiga vita ufisadi nchini humo.
Zuma anatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa dola milioni 16 za fedha za umma kwa ajili ya kuifanyia ukarabati nyumba yake binafsi iliyopo katika eneo la Nkandla, mashariki mwa nchi hiyo.
Mwaka 2014 Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Afrika Kusini, Thuli Madonsela alihukumu kwamba Rais Zuma alitumia vibaya ujenzi uliofanywa katika makazi yake binafsi huko KwaZulu-Natal na kumtaka kiongozi huyo arejeshe baadhi ya fedha za umma zilizotumika katika mradi huo.
Huku hayo yakijri, vyama vya upinzani nchini humo vikiongozwa na Democtratic Alliance vimeanzisha kampeni za kumuondoa madarakani Rais Zuma kufuatia uamuzi wa leo wa Mahakama ya Katiba.
Viongozi wa upinzani wanasema Zuma amepoteza itibari ya kuwa rais kwa kukiuka kwa makasudi katiba ya nchi.