Polisi 1400 wajiuzulu Kenya kwa kupunguziwa mishahara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41889-polisi_1400_wajiuzulu_kenya_kwa_kupunguziwa_mishahara
Maafisa 1,400 wa polisi wamejiuzulu wakilalamikia hatua ya Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) kupunguza mishahara yao.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 19, 2018 11:53 UTC
  • Polisi 1400 wajiuzulu Kenya kwa kupunguziwa mishahara

Maafisa 1,400 wa polisi wamejiuzulu wakilalamikia hatua ya Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) kupunguza mishahara yao.

Maafisa hao ambao tayari wamepokea mshahara wa Machi wameviambia vyombo vya habari kwamba mshahara wao umepunguzwa kwa hadi Sh26,000.

Wengi walioathiriwa ni wale walio na digrii na waliolemaa wakiwa kazini ambao walipunguziwa mshahara licha mahakama kuagiza serikali isitekeleze agizo la NPSC ambalo lilitolewa wiki iliyopita.

Wakati huo huo Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya, (KNCHR) leo Jumatatu imekemea vikali ripoti kwamba mshahara wa maafisa wa polisi umepunguzwa na kuitaja kuwa ni hatua isiyofaa. 

Bi Kagwira Mbogori

Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Kagwira Mbogori amesema Idara ya Polisi imekuwa ikitekeleza majukumu muhimu ya kudumisha amani na hatua hiyo itaathiri mno mageuzi ambayo yamekuwa yakiendelezwa na tume ya huduma kwa polisi.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Huduma kwa polisi Bw. Johnstone Kavuludi anasema: “Kuna maafisa ambao hawajawasilisha vyeti vya kuhitimu stashahada na shahada lakini wanapokea mshahara wa afisa wa cheo cha konstebo, na kwamba hao ndio wanaopambana nao.”