Mwanasheria mkuu mteule Kenya, Kihara Kariuki, ajitetea bungeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42026-mwanasheria_mkuu_mteule_kenya_kihara_kariuki_ajitetea_bungeni
Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Mwanasheria Mkuu nchini Kenya leo amefika bungeni na kujitetea akiahidi kulinda Katiba na Sheria za nchi na kuishauri serikali vilivyo, bila kushawishiwa kisiasa ama kwa njia nyingine yoyote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2018 11:22 UTC
  • Mwanasheria mkuu mteule Kenya, Kihara Kariuki, ajitetea bungeni

Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Mwanasheria Mkuu nchini Kenya leo amefika bungeni na kujitetea akiahidi kulinda Katiba na Sheria za nchi na kuishauri serikali vilivyo, bila kushawishiwa kisiasa ama kwa njia nyingine yoyote.

Jaji Kariuki ambaye amekuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa, akiwa mbele ya Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa, inayoongozwa na Spika Justin Muturi, kuhojiwa kuhusu mpango wake wa kikazi, alisema, “Ikiwa nitaidhinishwa, ninawahakikishia kuwa nitaelekezwa na Katiba. Afisi ya Mwanasheria Mkuu inawakilisha watu wa Kenya na sio chombo cha chama chochote cha siasa,” alisema Jaji Kariuki.

Jaji Kariuki pia aliahidi kukabiliana na ufisadi akisema kuwa atafanya vikao na afisi nyingine husika kama ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Idara ya Upelelezi (DCI) na hata Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) kuweza kubainisha changamoto ziko wapi, kuhusiana na kesi za ufisadi.

Jaji Kariuki alikuwa mbele ya Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa la Kenya

Kihara aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya mwanasheria  Githu Muigai kujiuzulu ghafla. Muigai amehudumu kama mkuu wa sheria kwa muda wa miaka 6 sasa.

“Nimepokea barua ya kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu Githu Muigai kwa kusononeka. Ninamshukuru kwa kazi aliyofanya kwa miaka sita na nusu. Nimempendekeza jaji Paul kihara Kariuki kuchukua nafasi yake.” Taarifa kutoka kwa ukurasa wa Rais Uhuru wa Twitter ilisema baada ya Muigai kujiuzulu.