DRC kususia kikao cha wafadhili Geneva; yasema UN inaiharibia jina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42100-drc_kususia_kikao_cha_wafadhili_geneva_yasema_un_inaiharibia_jina
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema haitashiriki mkutano wa wafadhili wake mjini Geneva, Uswisi kutokana na kile inachosema ni jina lake kuharibiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2018 02:57 UTC
  • DRC kususia kikao cha wafadhili Geneva; yasema UN inaiharibia jina

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema haitashiriki mkutano wa wafadhili wake mjini Geneva, Uswisi kutokana na kile inachosema ni jina lake kuharibiwa.

Mkutano huo unapanga kuchangisha dola bilioni 1.7 ambazo Umoja wa Mataifa umesema zinahitajika kukabiliana na maafa ya kibinadamu DRC.

Kaimu waziri mkuu  wa DRC Jose Makila amekubali kuwa nchi yake inakabiliwa na hali mbaya lakini amesema Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutoa misaada yanakuza kupita kiasi maafa ya nchi hiyo jambo ambalo limepelekea wawekezaji wasiwe na hamu ya kuwekeza katika nchi hiyo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibnuni lilionya kuwa hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeendelea kuwa mbaya na imefikia hatua ya kuwa janga kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa.

Raia wa DRC zaidi ya milioni 13 wanahitaji misaada ya kibinadamu wakiwemo watu milioni 7 na laki 7 ambao wana uhaba mkubwa wa chakula, imesema taarifa ya siri kwenye umoja wa Mataifa.

Rais Joseph Kabila

Baraza hilo limeeleza umuhimu wa kushughulikia tatizo la makundi yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo na kurejea wito wake wa kuwepo kwa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Serikali ya DRC imetangaza tarehe 23 ya mwezi Desemba mwaka huu kuwa tarehe rasmi ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, lakini hadi sasa bado haieleweki ikiwa rais Joseph Kabila atawania tena katika uchaguzi huo au la ili kutekeleza mapokezano ya madaraka kwa amani baada ya kumaliza mihula yake.

Umoja wa Mataifa umetangaza hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa katika ngazi ya 4, ngazi ya juu zaidi ya UN kuhitajika misaada ya dharura.