Jeshi la DRC laua waasi 13 Ituri
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuua waasi 13 katika mapigano yaliyojiri katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Ituri ni moja ya majimbo yanyokumbwa na mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hali ilizidi kuwa mbaya mkoani humo pale Rais Joseph Kabila alipoamua kuendelea kubakia madarakani baada ya muhula wake kumalizika mwaka 2016.
Msemaji wa Jeshi Jules Ngongo amesema mapigano yalijiri katika vijiji vya Jemi na Penyi katika eneo la Djugu. Aidha amesema mwanajeshi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika tukio hilo.
Kihistoria mkoa wa Ituri ni kati ya maeneo ambayo mapigano huibuka mara kwa mara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na muundo wake wa kikabila. Vita vya ndani vya DRC vya mwaka 1998 vilianza mkoani Ituri na kuendelea kwa muda wa miaka mitano ambapo watu wapatao milioni tano walipoteza maisha, wengi kutokana na njaa na magonjwa. Hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa kuwa yamkini DRC ikatumbukia tena katika vita vya ndani.
Hayo yanajiri wakati ambao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema haitashiriki mkutano wa wafadhili wake mjini Geneva, Uswisi kutokana na kile inachosema ni jina lake kuharibiwa.
Mkutano huo wa mwezi Aprili unapanga kuchangisha dola bilioni 1.7 ambazo Umoja wa Mataifa umesema zinahitajika kukabiliana na maafa ya kibinadamu DRC.
Kaimu Waziri Mkuu wa DRC Jose Makila amekubali kuwa nchi yake inakabiliwa na hali mbaya lakini amesema Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutoa misaada yanakuza kupita kiasi maafa ya nchi hiyo jambo ambalo limepelekea wawekezaji wasiwe na hamu ya kuwekeza katika nchi hiyo.