UN yahitaji $M 105 kuokoa maisha kwenye ukame Somalia
Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini Somalia yamezindua ombi la msaada wa dola milioni 105 kwa minajili ya kunusuru maisha na kujenga uthabiti wa zaidi ya watu milioni moja katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame kaskazini mwa Somalia
Ukame huo ambao makali yake yameongezwa na hali ya hewa ya El Niño, unaathiri maeneo ya majimbo ya Puntland na Somaliland, ambayo tayari yanakumbana na hali mbaya ya kibinadamu.
Taarifa ya Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa (OCHA), imesema watu wapatao milioni 1.7, sawa na ailimia 40 ya idadi nzima ya watu milioni 4.6 wanaoishi katika maeneo hayo, wanahitaji usaidizi wa kibinadamu na kuinuliwa kiuchumi.
Tayari, takriban watu laki nne wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
OCHA imesema iwapo usaidizi wa fedha hautapatikana haraka, madhara ya ukame huo yatakuwa makubwa zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa msimu ujao wa mvua umetabiriwa kuwa usio na mvua za tosha.