Miguna Miguna asafirishwa bila kujijua kutoka Kenya, ajikuta Dubai ghafla
Mwanasheria wa upinzani nchini Kenya na aliyeongoza shughuli ya kuapishwa kwa Kianara wa Muungano wa Upinzani (Nasa), Rais Odinga kuwa rais wa watu, Miguna Miguna amesafirishwa kwa ndege hadi mjini Dubai, bila kujitambua.
Hatia hiyo imejiri baada ya Miguna kuzuiliwa kuingia Kenya akitokea nchini Canada ambako alibaidishwa na serikali ya Nairobi siku chache baada ya kujiri tukio la kumuapishwa Odinga. Hata hivyo baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, alizuiwa na maafisa usalama wa serikali huku wakimpandisha ndege kwa nguvu suala ambalo alilipinga na hivyo kuamua kupiga kambi uwanjani hapo.
Hata hivyo wakati akiendelea kusubiria kuruhusiwa kuingia nchi hiyo na baada ya mahakama ya Kenya kutoa amri ya kutaka kuruhusiwa mwanasiasa huyo kuingia nchini, alisafirishwa kwa ndege majira ya usiku wa kuamkia leo bila ya yeye kujitambua. Mwanasiasa huyo ametimuliwa huku mzozo kuhusu uraia wake ukiwa bado unaendelea. Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook amesema kuwa, ameamka na kujikuta yuko mjini Dubai na kwamba anahitaji matibabu zaidi.
Amesema anafahamu kwamba kuna mpango wa kumpeleka London lakini anataka kupanda ndege ya kurejea tena jijini Nairobi. Kadhalika Miguna Miguna amesema kuwa amesindikizwa na ofisa wa idara ya ujasusi. Mawakili wa Miguna wamethibitisha suala hilo kwamba mteja wao ameondoshwa nchini humo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai. Habari za hivi punde zinaripoti kwamba, mwanasiasa huyo amelazwa hospitalini mjini Dubai kutokana na hali yake ya kiafya kuwa mbaya.