Njama za Israel za kueneza ushawishi wake barani Afrika
Gazeti la Kiingereza la Financial Times limetangaza habari kuhusu hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel za kujipenyeza na kupata waungaji mkono wapya barani Afrika, ili kuimarisha nafasi yake kimataifa.
Gazeti la Financial Times limeyasema hayo katika toleo lake la jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, baada ya utawala huo wa Kizayuni kudiriki kupoteza waungaji wake mkono barani Ulaya, hivi sasa umeanza kutafuta marafiki barani Afrika. Gazeti hilo limeongeza kuwa, licha ya mwezi Septemba mwaka jana 2015 Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuwasilisha muswada wa kuilazimisha Israel iruhu wakaguzi wa wakala huo kukagua vituo vyake vya nyuklia, lakini muswada huo haukupasishwa kutokana na nchi kadhaa za Afrika kujizuia kuupigia kura. Hii ni katika hali ambayo utawala huo wa Kizayuni, unamiliki makumi ya vichwa vya nyuklia na hadi hivi sasa unakaidi kutia saini mkataba wa kuzuia uzalishaji na usambazaji silaha hizo haramu na unakaidi pia mwito wa kimataifa wa kuruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kukagua shughuli zake za kuzalisha silaha angamizi za nyuklia. Hivi karibuni balozi wa utawala huo jijini Nairobi nchini Kenya alifanya safari jijini Dar es Salaam, Tanzania na kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Katika mazungumzo yao, balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Yahel Vilan alisema kuwa, Tel Aviv imeazimia kufungua uhusiano na Tanzania katika masuala mbalimbali pamoja na kufungua ubalozi wake jijini Dar es Salaam.